Swahili New Testament Bible

Romans 5

Romans

Return to Index

Chapter 6

1

 Tuseme nini basi? Je, twendelee kubaki katika dhambi ili neema ya Mungu iongezeke? 

2

 Hata kidogo! Kuhusu dhambi sisi tumekufa--tutaendeleaje kuishi tena katika dhambi? 

3

 Maana, mnajua kwamba sisi tuliobatizwa tukaungana na Kristo Yesu, tulibatizwa na kuungana na kifo chake. 

4

 Tulipobatizwa tuliungana na kifo chake, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka wafu kwa kitendo kitukufu cha Baba, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya. 

5

 Maana, kama sisi tumeungana naye katika kufa kama yeye, vivyo hivyo tutaungana naye kwa kufufuliwa kutoka wafu kama yeye. 

6

 Tunajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja na Kristo, ili hali ya dhambi iharibiwe, tusiwe tena watumwa wa dhambi. 

7

 Kwa maana, mtu aliyekufa, amenasuliwa kutoka katika nguvu ya dhambi. 

8

 Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye. 

9

 Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa kutoka wafu na hafi tena; kifo hakimtawali tena. 

10

 Hivyo, kwa kuwa alikufa--mara moja tu--dhambi haina nguvu tena juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu. 

11

 Hali kadhalika nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. 

12

 Kwa hiyo, dhambi isiitawale tena miili yenu ambayo hufa, na hivyo kuzitii tamaa zake. 

13

 Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni ninyi wenyewe kwa Mungu kama watu waliofufuliwa kutoka wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya uadilifu. 

14

 Maana, dhambi haitawatawala ninyi tena, kwani hamko chini ya Sheria, bali chini ya neema. 

15

 Basi, tuseme nini? Je, tutende dhambi ati kwa sababu hatuko chini ya Sheria bali chini ya neema? Hata kidogo! 

16

 Mnajua kwamba mkijitolea ninyi wenyewe kama watumwa na kumtii fulani, mnakuwa kweli watumwa wake mtu huyo--au watumwa wa dhambi, na matokeo yake ni kifo, au wa utii, na matokeo yake ni kukubaliwa kuwa waadilifu. 

17

 Ingawa mlikuwa watumwa wa dhambi zamani, sasa lakini--namshukuru Mungu--mmetii kwa moyo wote yale maazimio na mafundisho mliyopokea. 

18

 Mlikombolewa kutoka utumwa wa dhambi, mkawa watumwa wa uadilifu. 

19

 (Hapa natumia lugha ya kawaida ya watu kwa sababu ya udhaifu wenu wenyewe.) Kama vile wakati fulani mlivyojitolea ninyi wenyewe kutumikia uchafu na uhalifu kwa ajili ya uovu, vivyo hivyo sasa jitoleeni nafsi zenu wenyewe kutumikia uadilifu kwa ajili ya utakatifu. 

20

 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na uadilifu. 

21

 Sasa, mlipata faida gani siku zile kutokana na mambo yale ambayo mnayaonea aibu sasa? Maana, matokeo ya mambo haya ni kifo! 

22

 Lakini sasa, mmekwisha kombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mmekuwa watumishi wa Mungu; faida mliyo nayo sasa ni utakatifu, na matokeo yake ni uzima wa milele. 

23

 Kwa maana mshahara wa dhambi ni kifo; lakini zawadi anayotoa Mungu ni uzima wa milele katika kuungana na Kristo Yesu, Bwana wetu. 

Romans 7

 

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: