| Chapter 21 |
1 | Yesu alitazama kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya Hekalu, |
2 | akamwona pia mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo. |
3 | Basi, akasema, "Nawaambieni kweli, mama huyu mjane ametia zaidi katika hazina kuliko wote. |
4 | Kwa maana, wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi." |
5 | Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya Hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema, |
6 | "Haya yote mnayoyaona--zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa." |
7 | Basi, wakamwuliza, "Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani zitakazoonyesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?" |
8 | Yesu akawajibu, "Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: `Mimi ndiye`, na, `Wakati ule umekaribia`. Lakini ninyi msiwafuate! |
9 | Basi, mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado." |
10 | Halafu akaendelea kusema: "Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. |
11 | Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, kutakuwa na njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani. |
12 | Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu. |
13 | Hii itawapeni fursa ya kushuhudia Habari Njema. |
14 | Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea, |
15 | kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hivyo kwamba zenu hawataweza kustahimili wala kupinga. |
16 | Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti ninyi; na baadhi yenu mtauawa. |
17 | Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu. |
18 | Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea. |
19 | Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu. |
20 | "Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo mtambue ya kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa. |
21 | Hapo walioko Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani wasirudi mjini. |
22 | Kwa maana siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie. |
23 | Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa. |
24 | Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia. |
25 | "Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari. |
26 | Watu watazirai kwa sababu ya uoga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa. |
27 | Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi. |
28 | Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia." |
29 | Kisha akawaambia mfano: "Angalieni mtini na miti mingine yote. |
30 | Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. |
31 | Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka, mtatambua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia. |
32 | Nawaambieni hakika, kizazi hiki cha sasa hakitapita kabla ya hayo yote kutendeka. |
33 | Mbingu na dunia vitapita, lakini maneno yangu hayatapita. |
34 | "Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, Siku ile itawajieni ghafla. |
35 | Kwa maana itawajia kama mtego, wote wanaoishi duniani pote. |
36 | Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu." |
37 | Wakati wa mchana, siku hizo, Yesu alikuwa akifundisha watu Hekaluni; lakini usiku alikuwa akienda katika mlima wa Mizeituni na kukaa huko. |
38 | Watu wote walikuwa wanakwenda Hekaluni asubuhi na mapema, wapate kumsikiliza. |